KAMPALA,UGANDA

WIZARA  za Afya na Elimu nchini Uganda zimewasilisha ripoti yao kwa Rais  juu ya kupambana na Covid-19 ,na uamuzi wa mwisho kuhusu kufungua tena skuli  au kutofungua mwaka huu.

Waziri wa elimu ya juu Dk John Chrysostom Muyingo, alisema sasa wanangojea uamuzi wa Rais.

“Sasa tunasubiri uamuzi wa Rais ,yeye ndie atakaetangaza kufungwa na kufunguliwa tushampa taarifa zote ,anasubiri kupata uthibitisho kutoka kwa Waziri wa Afya.Kadri atakavyopata taarifa zote ndipo atatuambia hatua nyengine ya kuchukuliwa,”Mr Muyingo alisema.

Chama cha Uganda Peoples Congress (UPC) kiliibua wasiwasi juu ya kuongezeka kwa mimba za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za watoto wakiwemo wanafunzi wa skuli kutokana na kufungwa kwa skuli.

Shule na taasisi nyengine ni  maeneo yaliyofungwa mnamo Machi ili kuzuia  maambukizi ya ugonjwa huu.

Msemaji wa chama cha UPC Sharon Arach Oyat, aliitaka Serikali kuweka kipaumbele ulinzi wa wasichana kwa kuanzisha mifumo ya ukaguzi wa nyumbani.