TAMASHA la 25 la Utamaduni wa Mzanzibari lilifunguliwa rasmi juzi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi kwenye viwanja vya Mapinduzi Square ambapo kauli mbiu yake ni ‘Amani yetu ni matunda ya Utamaduni wetu’.
Tamasha hilo la kila mwaka lililoasisiwa na rais wa Awamu ya Tano, Dk.Salmin Amour, ni miongoni mwa hazina ambazo Zanzibar likiwa taifa huru, linajivunia kuliangana na aina ya utamaduni iliyonao.
Tunachukuwa nafasi hii kulitakia kila la heri tamasha hilo la wiki moja litakalofanyika Unguja na Pemba. Zanzibar kama yalivyo mataifa mengine, imebarikiwa kuwa na historia kubwa hasa kwenye suala zima la utamaduni, ambao umekuwa kielelezo halisi cha urithi kutoka kizazi kimoja hadi chengine.
Utamaduni umekuwa na faida kubwa kwa wananchi na jamii kwa ujumla, japokuwa imekuwa vigumu kwa wengine kulitambua hili, kwa sababu wanapotekeleza utamaduni wao hufanya kwa kujifurahisha zaidi.
Moja ya faida kubwa ya utamaduni ni ile ya kiuchumi, ambapo lipo kundi la watalii wanaofunga safari kutoka nchini kwao na kuja visiwani hapa kuja kujifunza, kuziona na kuzishuhudia mila, silka na utamaduni wetu.
Kwa bahati nzuri baadhi ya watalii hao hufikia hata kuiga utamaduni huo, kwa mfano mara ngapi tumewashuhudia wazungu wakipaka piko ambayo haina madhara kama michoro ya ‘tattoo’ wanazojichora.
Lakini pia wapo watalii wanaotoka katika nchi zao na kuja kuangalia tu majengo yetu hasa yaliyoko Mji Mkongwe na kwenye hifadhi nyengine kwa sababu majengo hayo ni kielelezo cha utamaduni wetu.
Hata hivyo cha kusikitisha ni kwamba upande wa ngoma zetu za asili ambazo ni sehemu muhimu ya utamaduni wetu hivi sasa zimeanza kupotea.
Ngoma zetu za asili zilizokuwa zikichezwa, kupigwa na kuimbwa na wazee wetu katika mitaa na vijiji vyetu, baadhi leo hii hazipo tena, huku vijana wanaochipukia wakionekana kujikita zaidi na nyimbo za kimagharibi.
Kila nyumba unayopita vijana wanaimba bongo ‘fleva’, staili ya muziki ambayo ni zao la aina za nyimbo kutoka nchi za magharibi.
Vyombo vyetu vya habari vimezisahau kabisa ngoma zetu za asili kama kinyakunyaku, mkugo, bomu, mdundiko, boso, maumbwa, gonga, mkurungu, kirumbizi, gombe sugu, ndarandara, vanga, msondo na hata mchezo wa ng’ombe.
Kwa uchache kabisa tumebakiwa na ngoma kama vile kibati na msewe tena kwa sababu serikali imekuwa ikihahamisha kwenye sherehe rasmi,hata beni nalo hivi sasa limekuwa adimu.
Kwenye muziki wa taarabu huko hakuzungumziki, kwa sababu taarab inayopigwa hivi sasa na kuhamasisha kwenye vyombo vya habari ni ile tunayodiriki kusema imekosa aina fulani wa taarab iliyokuwa ikipigwa visiwani hapa.
Taarab ya leo inapopigwa haina tofauti sana na muziki wa dansi kwa maana kwamba lazima kijasho kikutoke ukienda katika muziki huo, na kama inachezwa kwenye uwanja wa vumbi ukitoka ukumbini ukajitie maji la si hivyo usingizi huwezi kuupata.
Taarab ya asili tunayoizungumza ni ile ambayo kanzu ama gauni la mwenye kwenda kwenye muziki huo, likitiwa udi au mafuta mazuri harufu yake haiwezi kupotea hata pale unaporudi nyumbani.
Tukizungumzia yale yaliyomo kwenye mashairi tena hapo ndio huwezi kusema, kwa sababu umetumika usanii mkubwa wa kuisarifu fasihi, jambo ambalo ni tofauti kubwa na nyimbo za taarab ya kisasa.