SANAA,YEMEN

SPIKA wa Bunge la Yemen amesema kuwa uhalifu unaofanywa na Saudi Arabia na washirika wake nchini humo pamoja na kuendelezwa muungano wa nchi hiyo haviwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.

Mohammed Hussein al-Aidarous aliwatumia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,Antonio Guterres na mjumbe wa umoja huo katika masuala ya Yemen,Martin Griffiths na kueleza hali halisi kuhusu mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Saudi Arabia na washirika wake huko Yemen na vathari za mashambulizi hayo kwa maisha ya raia wa nchi hiyo.

Hussein al-Aidarous alisema kuwa, uhalifu unaofanywa na muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen na hatua ya wavamizi hao ya kuzuia meli zinazobeba nishati na chakula kutia nanga katika bandari za Yemen ni jinai na uhalifu mkubwa ambao hauwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.

Alisisitiza kuwa,vikwazo vya kidhalimu dhidi ya watu wa Yemen vinakwamisha jitihada za kupeleka chakula nchini humo na kuzidisha machungu na mashaka ya Wayemeni.

Al-Aidarous aliongeza kuwa, kimya cha jamii ya kimataifa mbele ya uhalifu huo kinazidisha mashaka na machungu hayo.

Spika wa Bunge la Yemen aliitaka jamii ya kimataifa kudumisha mashinikizo dhidi ya Saudi Arabia na washirika wake katika vita vya Yemen kwa shabaha ya kuruhusu shehena za meli zinazobeba mafuta, chakula na dawa kutia nanga katika bandari za Yemen.