NA ASIA MWALIM
MAMLAKA ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), imesema itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha matukio yanayohusisha vitendo vya rushwa yanapungua nchini.
Ofisa Elimu kwa Umma kutoka ZAECA, Harrieth Limo, alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye viwanja vya maonyesho ya tatu ya wakulima ya nane nane Dole.
Alisema mamlaka hiyo inahusika kwenye mapambano ya rushwa, hata hivyo kuna umuhimu mkubwa wa jamii kuwa na elimu dhidi ya rushwa ili waweze kuwaripoti pale vitendo hivyo vitakapojitokeza.
Alisema wapo baadhi ya watendaji wanakwenda kinyume na sheria za kazi, hivyo ni vyema wananchi kuwafichua bila kujali cheo kwani kufanya hivyo itasaidia kuwa na watumishi bora.
Ofisa huyo alisema mamlaka hiyo imejipanga kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa ngazi tofauti, ikiwemo maeneo ya kazi ya sekta na taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi ili kupunguza mianya ya rushwa.
Aidha alisema ZAECA inaendelea na uthibiti wa matukio ya rushwa kwa kuyafanyia uchunguzi malalamiko wanayoyapata kutoka kwa wananchi, hivyo huyatafutia ufumbuzi malalamiko hayo ikiwemo kuzifikisha mahakamani kesi zao.