NA ZAINAB ATUPAE
KAMATI Tendaji ya Chama cha Soka Mkoa wa Mjini Magharibi, imesema, katika hakikisha wanapambana na rushwa kwa waamuzi wao, wameamua kukutana na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), ili kuhakikisha wanafutilia mechi zilizobakia.

Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili huko Ofisini za ZFA wilaya ya Magharibi ’B’ Unguja, Katibu wa cha hicho, Ahmada Haji Khamis, alisema, lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha wanaondoa rushwa ambayo inatajwa kwa waamuzi wao.

Alisema, wanaamini mazungumzo waliofanya na ZAECA yatafikia malengo yao, kuanzia ligi za mkoa hadi wilaya na kuleta taswira bora ya soka nchini.
Alisema mbali na kuzungumza na ZAEZA walikutana pia na waamuzi pamoja na makamisaa wa ligi kuhakikisha wanatoa tahadhari juu ya rushwa viwanjani.

Hata hivyo, katibu huyo, alikiri kuwa katika soka rushwa ipo na imeonekana kuwa sugu na katika kuiepusha na kuiondosha, ZAECA watakuwa wakifuatilia mechi zote.
Alisema kutokana na mechi zilizobakia kuwa ngumu wamelazimika kuzungumza na vyombo vya usalama ili kuepusha vurugu ambazo zinaweza kujitokeza viwanjani.

Hivyo aliwataka mashabiki kujitokeza kuangalia mechi hizo ili kuleta hamasa badala ya vurugu zisizotarajiwa.