NA MWAJUMA JUMA

CHAMA Cha Mpira wa Wavu Zanzibar (ZAVA), kimeendelea kuwaomba wadau wa michezo nchini, kujitolea kusaidia chama hicho kwa kuwapatia udhamini kwenye ligi zao.

Ombi hilo limetolewa na Katibu Msaidizi wa chama hicho Eutist Mwakanjuki alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi, katika kuelekea ligi kuu ya Zanzibar ya mchezo huo inayotarajiwa kuanza Agosti 18 mwaka huu, kisiwani Pemba.

Alisema  ligi yao inakaribia kuanza lakini changamoto kubwa ambazo mpaka sasa inawakabili ni ukosefu wa udhamini wa ligi tatizo ambalo ni sugu.

Alieleza kuwa kila mwaka huandika barua kwa taasisi mbali mbali kuhusu kupatiwa ufadhili, lakini hawafanikiwi hali ambayo inazifanya hata klabu kukosa hamu ya kushiriki ligi hiyo.

“Mara zote Zanzibar hutoa timu tatu ikiwemo Mafunzo, Nyuki na Polisi,lakini mara hii Polisi imeshindwa kushiriki kwa sababu ambazo wanazijuwa wenyewe, lakini na hilo pia la kutokuwa na wafadhili linachangia.

Hivyo aliwaomba wahisani na wadau mbali mbali wa michezo kujitokeza kusaidia chama chao, katika kuwapatia ufadhili wa aina yoyote iwe kwa vifaa vya waamuzi, zawadi za wachezaji na hata maji.

Alieleza kuwa wamekuwa katika wakati mgumu wanapoendesha michuano yao kutokana na kukosa ufadhili, ambao kupatikana kwake kutachangia kwa kiasi kikubwa kuinua mchezo huo.