NA LAYLAT KHALFAN
MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA), Mussa Ramadhan Haji, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ina azma ya kuwaunganisha wananchi wa Unguja na Pemba kwa kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia majumbani badala ya kutumia mifereji ya nje.
Mkurugenzi huyo aliyasema hayo Ofisini kwake Mabluu wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wa gazeti hili, kuhusiana na mikakati ya huduma ya maji safi na salama katika kisiwa hichi kwa kipindi kijacho.
Alisema kwa kipindi wanachoelekea cha ilani ya CCM 2020 /2025 , utegemezi wa visima binafsi kwa maeneo yote ambayo yana makaazi ya kudumu itakuwa basi, huku tegemeo lao kwa wananchi wa Zanzibar ni kuona hakuna mtu ambae atakosa huduma hiyo nyumbani kwake mjini na vijijini.
Mussa alisema kwa wale ambao wamejitenga mbali peke yake watakuwa hawana uwezo wa kuwasogezea huduma hiyo na badala yake wataruhusu kuchimba visima, ili kupata huduma hiyo.
“Visiwa vidogo vidogo vyote tutavikamilisha wakati Pemba kimebaki kisima kimoja ambacho kimefikia asilimia 70 kukamilka na sasa tupo karibu kuunga pampu, ili kutoa huduma kama ilivyokusudiwa,” alisema.