NA KHAMISUU ABDALLAH

WAKALA wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA), imewasisitiza wanandoa kwenda kujisajili na kupata vyeti rasmi vya ndoa ili kujiepusha na changamoto mbalimbali hasa za mirathi.

Imeelezwa kuwa karatasi ya ndoa inayotolewa na kadhi wakati wa kufunga ndoa sio cheti rasmi, bali ni uthibitisho unaotolewa kwa wanandoa hao.

Ombi hilo limetolewa na Ofisa Usajili wa Mamlaka hiyo Hamid Haji Makame wakati akizungumza na Zanzibar Leo huko Dole.

Aidha alisema pamoja na mamlaka hiyo kutoa elimu kupitia vyombo vya habari bado wananchi wengi hawana muamko wa kusajili vyeti vya ndoa na kujua karatasi wanayomiliki ndio cheti rasmi cha ndoa jambo ambalo sio sahihi.

“Wengi wao hawajui kwani wakifika hapa wanashangaa kwamba kuna cheti rasmi cha ndoa na tunawaelimisha kufika katika mamlaka yetu ili kupatiwa cheti rasmi kwa taratibu tulizoweka”, alisema.

Alisema mara nyingi wale wanaokwenda kujisajili na kutaka cheti cha ndoa ni wale wanaokwenda nje ya nchi tofauti na wananchi wa kawaida.

“Wengi wanaotaka kusafiri wanapodaiwa cheti cha ndoa ndio wanaokuja lakini waliokuwepo katika jamii muamko bado mdogo,” alisema.

Alifahamisha kuwa cheti cha ndoa ni muhimu kwa wanandoa ikiwemo katika mirathi kwa kutambulika mwanandoa halali na kusaidia watoto katika mambo ya mirathi pamoja na kupata hati ya kusafiria.

Hivyo, aliwataka wananchi kufika katika mamlaka hiyo kwa ajili ya kujisajili na kupatiwa cheti rasmi cha ndoa ili kujiepusha na matatizo yasiyokuwa ya lazima.

Sambamba na hayo, alisema mamlaka hiyo itaendelea kutoa elimu ili kuona wananchi wanahamasika katika kusajili vyeti mbalimbali vikiwemo vya ndoa.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka hiyo, Shaaban Ramadhan Abdalla, aliwaomba wananchi kuitumia siku ya usajili kwa kusajili ndoa, talaka, vizazi na vifo na vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi.

Alisema, serikali imeweka mamlaka hiyo ili kuwahudumia wananchi kwa kuwapatia hati mbalimbali ambazo zitawasaidia katika harakati mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo.