NA HAFSA GOLO

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) inatarajia kufanya mafunzo maalumu kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, kuwakumbusha juu ya sheria ya uchaguzi na namna ya kuripoti habari za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Thabit Idarous Faina, alieleza hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake Maisara mjini Unguja na kueleza kuwa mafunzo hayo yatafanyika baadae mwezi huu.

Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuhakikisha wanahabari wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi sambamba na kutambua matakwa ya sheria za uchaguzi ili kuondoa changamoto za kiutendaji.

“Vyombo vya habari ni miongoni mwa wadau na taasisi muhimu zenye kutoa taaluma kwa jamii ya ndani na nje ya nchi juu ya hatua na mwenendo mzima wa uchaguzi hivyo ni vyema tukawakumbusha juu ya wajibu na majukumu yetu kama wadau ili kuwa na uchaguzi ulio bora zaidi,” alieleza Faina. 

Alisema ZEC itahakikisha inasimamia sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika upatikanaji wa fursa sawa kwa wadau wote kutokana na umuhimu wao lakini pia miongozo na matakwa ya sheria ya uchaguzi.

Aidha Mkurugenzi huyo alitumia nafasi hiyo kuvikumbusha vyama vya siasa kuzingatia ratiba ya uchaguzi iliyotolewa na tume hiyo na kukamilisha kwa wakati michakato ya kuwapata wagombea wao.

“Sisi (ZEC) tumeshatoa ratiba na hatutarajii kuibadili kwa sasa hivyo vyama ni lazima viizingatie ratiba hiyo katika ratiba zao lakini pia kuzingatia taratibu za kisheria wakati wa zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu na nyengine zilizopo mbele yetu,” aliongeza Faina.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuondosha malalamiko yasiyo ya lazima. Aliwahakikishia wanasiasa na wananchi kwa jumla kwamba tume hiyo ipo huru na itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa misingi ya haki na uwajibikaji.

Akizungumzia watu wenye mahitaji maalumu, Faina alisema tume imewaandalia vitambulisho maalumu vitakavyowaruhusu kupiga kura bila ya kukaa foleni na wakati wowote vitapelekwa katika jumuiya zao.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na tume hiyo hivi karibuni, zoezi la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi wa wagombea litafanyika kuanzia Agosti 26 hadi Septemba 9 wakati uteuzi wa wagombea utafanyika Septemba 10.

Kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo zinatarajiwa kuanza Septemba 11 hadi Oktoba 26 mwaka huu zoezi ambalo litafuatiwa na upigaji kura ya mapema Oktoba 27 utakaohusisha watendaji wa baadhi ya vyombo na watendaji wa tume watakaohusika na usimamizi wa uchaguzi huo utakaofanyika na kufuatiwa na uchaguzi mkuu Oktoba 28 mwaka huu.