NA JAALA MAKAME HAJI, ZEC

TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imewataka wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya jimbo walioteuliwa kusimamia Uchaguzi katika Majimbo ya Zanzibar kuifanya kazi hiyo kwa kuzingatia Sheria na maelekezo waliyopewa na Tume.

Mjumbe wa Tume hiyo, Dk. Kombo Khamis Hassan, alitoa ushauri huo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa Wasaidizi wasimamizi wa uchaguzi kwa Majimbo ya Unguja yaliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil Kikwajuni jijini Zanzibar.

Dk. Kombo, alisema Tume imekuwa ikiendelea kuchukua juhudi mbali mbali za kuwakutanisha Wadau wa uchaguzi wakiwemo Vyama vya Siasa, Waandishi wa habari, Asasi za Kiraia na Wadau wa kutoka katika makundi yenye mahitaji maalum kwa lengo la kuona uchaguzi wa mwaka 2020 unafanyika kwa kufuataa misingi ya Kidemokrasia na kudumisha Amani na utulivu hata baada ya Uchaguzi.

Akifunga Mafunzo hayo Mjumbe wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Kanali Mstaafu, Fetehe Saad Mgeni, aliwataka Wasimamizi wa uchaguzi na Wasaidizi Wasimamizi kuhakikisha kila mwenye haki ya kuchagua na kuchaguliwa anapata haki yake, ili kuweka mustakbali mzuri wa uchaguzi.Mkuu wa mwaka 2020.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Khamis Issa Khamis, alisisitiza kuwa kazi za Uchaguzi zinahitaji umakini wa hali ya juu kati hatua zote muhimu ikiwemo hatua ya ujazaji wa fomu za matokeo ya Uchaguzi, utunzaji wa vifaa, kuhesabu kura na kutangaza matokeo.