NA MWINYIMVUA NZUKWI

MWENYEKITI wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jaji Mkuu Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid amewakumbusha waandishi wa habari na vyombo vya habari wajibu wa kuzingatia maadili ya kazi yao ili kufanikisha uchaguzi mkuu ujao.

Akifungua mafunzo kwa wahariri na waandishi wa habari katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni mjini Zanzibar, Jaji Mahmoud alisema mafanikio ya uchaguzi huo unategemea ushiriki wa wadau wote vikiwemo vyombo vya habari.

Alisema ili kuepusha mkanganyiko na vurugu katika jamii, wanahabari wanapaswa kutumia kikamilifu taaluma yao kusaidia jamii kuwa na uelewa katika kila hatua ya uchaguzi.

“Katika kutekeleza majukumu yenu, ni vyema kabla ya kuruhusu habari kwenda hewani mkajiridhisha juu ya taarifa hiyo kama haiendi kinyume na sheria au kanuni za uchaguzi au kuleta vurugu,” alisema Jaji Mahmoud.

Aidha alivipongeza vyombo hivyo kwa kufanya kazi kwa karibu na tume hiyo jambo lilipelekea kupatikana kwa taarifa nyingi za uchaguzi kwa jamii.

Akiwasilisha mada ya sheria za uchaguzi, Mwanasheria wa tume hiyo Khamis Issa Khamis alisema kwa mujibu wa sharia hiyo ni makossa kwa chombo cha habari kutangaza matokeo kabla ya taarifa rasmi ya tume.