NA HAFSA GOLO

MGOMBEA nafasi ya urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wakulima (AFP), Said Soud Said, amesema iwapo wazanzibari watampa ridhaa kwa kumchagua katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, atahakikisha anadumisha utu wa mwananchi wa Zanzibar.

Soud alieleza hayo jana kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) zilizopo Maisara mjini Zanzibar, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa fomu ya uteuzi na Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Mstaafu, Hamid Mahmoud Hamid.

Alisema endapo wananchi watampa ridhaa jambo la msingi atakalolisimamia ni kuhakikisha heshima na utu wa mwananchi wa Zanzibar unapewa kipaumbele.

“Silka, mila na utamaduni za mzanzibari ni miongoni mwa mambo muhimu nitakayoyasimamia, mambo hayo ndiyo yanayompatia heshima na utu wake mwananchi wa Zanzibar”, alisema Soud.

Aidha alisema kuwa jambo jengine atakalolisimamia ni kuhakikisha anainua maslahi ya waandishi wa habari ambao aliwataja kama watu wa muhimu na wenye mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi.

Aidha alisema pamoja na utekelezaji wa mipango hiyo pia atahakikisha anaendeleza mazuri yote yaliyowachwa na serikali ya awamu ya saba kwa kusimamia uchumi.

Alibainisha pamoja na kwamba anawania nafasi hiyo kupitia chama cha upinzani, lakini anaamini Chama cha Mapinduzi, ndicho chenye dira sahihi ya kuleta maendeleo na mageuzi ya kiuchumi.

Hivyo, alisema miongoni mwa jambo muhimu litalokuwa kipaumbele katika uongozi wake ni pamoja na kusimamia amani na utulivu iliyoimarika katika uongozi wa serikali na kufikia malengo yaliyowekwa kwa maslahi ya wananchi.

Mapema Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud kabla ya kumkabidhi fomu mgombea huyo alimtajia miongoni mwa masharti ambayo mgombea hairuhusiwi kujihusisha ikiwemo suala  la rushwa.