NA MADINA ISSA

KAIMU Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Mjini, Haji Hassan Khamis, amewataka wataochukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuongoza kuwa makini katika kujieleza ili kuepuka usumbufu hapo baadae.

Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kuanza kwa zoezi la kumkabidhi fomu, katika  Ofisi ya Tume hiyo Maisara Mjini Unguja.

Alisema endapo fomu zikirejeshwa mapema zinasaidia kukaguliwa na endapo itakuwa amejaza kimakosa atarejeshewa na kujaza tena siku tatu kabla ya zoezi hilo kufungwa ili kuweza kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza katika fomu ikiwemo kukosea kujaza.

“Tunajua binaadamu anaweza kukosea hivyo kurejesha mapema kunasaidia kuzikagua vizuri na endapo tukibaini kuwa zinamapungufu tunaweza kumrejeshea kwa ajili ya marekebisho mapema na sio kusubiri siku ya mwisho kuleta fomu hizo huwa hana muda tena” alisema.

Alisema kuwa zoezi hilo limeanza Agosti 12, na hadi sasa linaendelea vizuri na hakuna tatizo lolote lilojitokeza na wagombea wanaendelea kujitokeza kuchukua fomu hizo kwa mujibu wa chama.

“Bado mapema siwezi kutaja vyama vilivyokuwa vishajitokeza kuchukua fomu ila zoezi linakwenda vizuri kama lilivyopangwa” alisema.

Sambamba na hayo, alifahamisha kuwa endapo mgombea nafasi ya Ubunge atapata asilimia 10 za kura zake jimboni atarejeshewa fedha zake alizozitoa katika uchukuaji wa fomu hiyo.