NA MWANDISHI WETU

SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF), limefungua dirisha la usajili na uhamisho wa wachezaji kwa msimu wa 2020/21, likitarajiwa kufungwa Septemba 19, mwaka huu.

Dirisha hilo la usajili limefunguliwa kwa timu za Ligi Kuu ya Zanzibar kwa upande wa wanaume, Ligi Kuu ya Wanawake, Ligi ya Mikoa pamoja na Ligi za Wilaya.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mashindano wa ZFF, Ali Mohmmed Ameir, amesema msimu huu klabu zitasajili kwa njia ya kielektroniki badala ya kujaza fomu kwa mkono kama ilivyozoeleka kwa misimu ya iliyopita.

Alisema ingawa kwa sasa njia hiyo italeta changamoto kwa baadhi ya klabu, lakini shirikisho hilo litazidi kutoa elimu ili kila klabu iweze kufanya usajili kwa wakati kwa kutumia njia ya kielektroniki.

Aidha, amezitaka klabu kufanya usajili kwa wakati uliowekwa na ZFF ili kuepusha usumbufu ambao unaweza kujitokeza mara kwa mara katika kipindi hiki hususan kwa baadhi ya timu kushindwa kusajili kwa wakati.