NA ABOUD MAHMOUD

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) limeshauriwa kwenda na wakati na kufuata kalenda ya FIFA na CAF ili kuweza kuendesha soka kama inavyotakiwa.

Hayo yamesemwa na kocha wa klabu ya Pulling Land inayoshiriki ligi daraja la pili Wilaya ya Mjini, Yussuf Abdulrahman Chunda wakati alipokutana na mwandishi wa habari hizi viwanja vya Mnazi Mmoja.

Chunda alisema hivi sasa timu zote duniani za mchezo wa soka ikiwemo Tanzania Bara zimemaliza ligi na usajili kwa wachezaji umeanza, lakini kwa upande wa Zanzibar bado hawajifikia hatua hiyo jambo ambalo linarudisha nyuma mchezo huo.

Alisema kufanya hivyo kunaonesha kurudisha nyuma hadhi ya mchezo wa soka visiwani humu, kwani dunia nzima hivi sasa inatizama msimu ujao wa ligi.

“Naiomba ZFF ibadilike iangalie kalenda FIFA na CAF sio kubaki nyuma kila siku,wenzetu wamemaliza lig, sisi bado ndo kwanza tunaendelea jambo ambalo sio zuri,”alisema.

Chunda alisema mpaka hivi sasa Zanzibar bado inaendelea na ligi ikiwemo ile ya daraja la pili, pamoja na kanda na pia ligi ya nane bora inatarajiwa kuanza jambo ambalo kinyume na utaratibu wa soka.

Alisema kwamba kuendelea kwa ligi katika kipindi hiki ambapo haijulikani itamaliza lini, kunasababisha wachezaji wengi kukosa kusajiliwa katika timu nyengine za Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Aidha kocha huyo alilitaka shirikisho hilo kuangalia kwa kina tatizo hili ili kuondosha usumbufu kwa wachezaji wanaotaka kwenda klabu nyengine na pia kwenda sawa na kalenda.