NA ZAINAB ATUPAE
RAIS wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) Seif Kombo Pandu, amesema lengo la kutoa mafunzo kwa makocha wanaofundisha walinda milango, ni kuhakikisha wanakuza na kuendeleaza vipaji vya walinda milango hao.
Akizungumza na gazeti hili huko uwanja wa Mao Zedong’s Rais huyo,alisema mafunzo hayo yatasaidia kukuza vipaji na kuleta maendeleo ya soka lao.
Alisema wanaamini kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutapatikana mabadiliko makubwa kwa walinda milango, ambapo kwa miaka mingi hawajapata nafasi hiyo.
Alisema zaidi ya makocha 30 wanaofundisha walinda milango kutoka timu mbali mbali, wanapatiwa mafunzo hayo.
Seif alisema amefarajika sana kwani makocha wamejitokeza kwa wengi,hivyo aliwataka wale ambao hawajabahatika kupata nafasi mara hii, kusubiri msimu mwengine yatakapotolewa mafunzo mengine.
Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo kocha Salehe Machupa,aliwataka makocha hao kuyafanyia kazi mafunzo waliopatiwa kwa lengo la kuleta mabadiliko ya soka la Zanzibar kama Shirikisho linavyotaka.
Alisema anamini kuwa mafunzo hayo yatatoa vipaji vizuri vya walinda milango katika timu zao.