NA MWAJUMA JUMA
KITENDAWILI cha timu ipi itapanda daraja kati ya timu za Black Sailor, Uhamiaji na Taifa ya Jang’ombe, kitateguliwa leo, wakati Black Sailor na Uhamiaji zitakaposhuka dimbani.
Hatua hiyo imekuja kutokana na mfungamano wa karibu wa pointi kwa timu hizo tatu, ambazo zinawania nafasi hiyo kwa upande wa Unguja, ambapo Black Sailor ikishinda itakuwa imejihakikishia kupanda ligi kuu kwa kufikisha pointi 50 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote.
Kwa upande wa Uhamiaji ambayo ipo nafasi ya pili ya msimamo wa ligi hiyo ina pointi 45, iwapo itashinda itafikisha pointi 47 na itabakisha mchezo mmoja.
Timu ya Taifa ya Jang’ombe wao wanaingia katika kinyang’anyiro hicho kwa kuangalia mwezi, kwani hivi sasa timu hiyo ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45, wamebakisha mchezo mmoja dhidi ya Uhamiaji.
Hivyo mchezo wa leo ambao utachezwa kwenye uwanja wa Mao Zedong saa 10:00 za jioni, matokeo yake ndio yatakayotoa taswira ya timu ipi itakuwa bingwa.
Kocha wa timu ya Black Sailor Juma Awadhi akizungumza na mwandishi wa habari hizi alisema,wamejipanga kupambana ili kuibuka na ushindi utakaowawezesha kupanda daraja.
Hata hivyo alisema mpira una matokeo matatu ambayo moja kati ya hilo linaweza kutokea, lakini kwa upande wake wamewaandaa vyema wachezaji wao kwa ajili ya kupambana.
Hivyo aliwataka wachezaji wake kutambua umuhimu wa mchezo huo ambao ndio utakaowawezesha kufikia malengo yao.
Nae kocha wa Uhamiaji Kijo Nadir Nyoni alisema kuwa lolote katika mpira linaweza kutokea na wao wamejipanga kwa ajili ya kwenda kutoa ushindani ili waweze kushinda.
Alisema mpira ni mchezo wa makosa ambapo linapotokea linakuwa faida kwa mpizani wake, hivyo kwa namna ambavyo wamejiandaa wanataka washinde ili kuwa na matumaini ya kupanda daraja.
“Bado tuna wakati mgumu kwenye mchezo huu, ingawa tunamjiandaa vizuri, lakini kila mmoja ana umuhimu mkubwa na mchezo huu, ili kujiweka katika mazingira mazuri”, alisema Kijo.
Mchezo kati ya wawili hao umepokelewa kwa hisia kubwa na mashabiki na wapenda soka na wengi wao kuwa na matumaini ya kuwa kutakuwa na ushindani wa hali ya juu.