NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), imepunguza kiwango cha utozaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 15.

Meneja Uhusiano, Huduma kwa Walipa Kodi Shaaban Yahya Ramadhani aliyasema hayo katika mafunzo yaliyowashirikisha waandishi wa habari juu ya marekebisho ya sheria za kodi kwa mwaka 2020/2021 yaliyofanyika katika ofisi za ZRB Mazizini.

Alisema marekebisho hayo yametiwa saini rasmi Juni 29 na kuanza kutumika rasmi kuanzia Julai 1 mwaka huu.

Alifahamisha kuwa serikali pia imefanya mabadiliko katika jadueli la pili la kodi hiyo kwa kuongeza baadhi ya vifaa vya uvuvi ambavyo vimesamehewa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).

Alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni pamoja na nyavu, ndoano, maboya, mashine za uvuvi na boti zote zinazozidi mita 18 na kuendelea.

“Kwa boti za kawaida ambazo zipo chini ya mita 18 hizi zitaendelea kulipa VAT (kodi ya ongezeko la thamani) kama kawaida,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema katika mabadiliko hayo serikali pia imebadilisha kiwango cha ada ya usajili wa mtu kwa kodi ya ongezeko la thamani kutoka shilingi milioni 30 hadi shilingi milioni 50.

Akizungumzia sheria ya ushuru wa mahoteli, alisema marekebisho yamefanyika katika kifungu cha 3 kwa kufuta kifungu cha kwanza (1) ambapo marekebisho yamelenga kuweka kiwango kipya cha kutoza katika mahoteli cha asilimia 12 na kufuta kiwango cha asilimia 18 kilichokuwepo awali.

Ofisa Shaaban alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuleta ufanisi katika ukusanyaji wa mapato na kufikia ulipaji kodi wa hiari kwa wafanyabiashara na kusimamia kodi za serikali.

Ofisa Uhusiano wa bodi hiyo Badria Attai Masoud alisema serikali imekuwa ikifanya mabadiliko ya sheria za kodi kila mwaka kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.

Hivyo, aliwasisitiza wananchi na wafanyabiashara kwa ujumla wasidharau wanapofikiwa na bodi hiyo kwani ZRB ina lengo la kuona wanashirikiana pamoja kuhakikisha serikali inapata mapato yake kama ilivyokusudia.

“Wasidhani mabadiliko haya yanakuja tu, sheria zinabadilishwa kwa yale maoni na mapendekezo yanayotolewa kwetu, tunapowaita au kuwafikia walipo matunda yake ndio haya,” alibainisha.

Kwa upande wake Ofisa Elimu kwa Walipa Kodi wa Bodi hiyo, Raya Suleiman Abdalla, alisema katika kuona kila mlipa kodi na wafanyabiashara yanawafikia mabadiliko hayo, ZRB imeshaanza kutoa elimu kupitia vyombo vya habari na kuwafikia wananchi maeneo ya mikusanyiko ikiwemo katika masoko.

Sheria zilizofanyiwa marekebisho hayo ni pamoja na sheria ya usimamizi wa kodi (TAPA), sheria ya kodi ya ongezeko la thamani (VAT), sheria ya ushuru wa hoteli, sheria ya kodi ya majengo pamoja na sheria ya rufaa za kodi Zanzibar.