Yaelekeza namna ya kufanya malipo

NA KHAMISUU ABDALLAH, LAILA KEIS

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imeiagiza Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) kuhakikisha hawapokei malipo yoyote ambayo hayana namba maalum (control number) yanayofanywa na taasisi za serikali.

Kauli hiyo ilitolewa na meneja Uhusiano, Huduma kwa Walipakodi, Shaabani Yahya Ramadhan, wakati akizungumza na wahasibu na wasaidizi wahasibu wa taasisi za serikali katika ukumbi wa bodi hiyo Mazizini.

Alisema wahasibu wa taasisi za serikali ikiwemo mashirika na idara wanaofanya malipo katika bodi hiyo lazima kuhakikisha wanapatiwa namba maalum ya malipo ili kuepusha usumbufu usiokuwa wa lazima.

Aidha alisema ikiwa wahasibu watafanya malipo bila ya kuwa na namba maalum basi malipo yao hayatahesabiwa kama malipo.

Alisema malipo yoyote yanayofanyika serikalini katika mfumo unaotumiwa na Wizara ya Fedha kufanya malipo IFIMS, basi lazima yaambatane na namba maalum ya malipo.

Meneja huyo, alisema serikali imeweka utaratibu huo kuona malipo yote yanayofanywa basi yafanywe kwa kutumia namba hiyo ili kuondosha changamoto mbalimbali za kifedha.

Aidha alisema lengo la kuanzishwa namba hiyo maalum ni kuirahisishia serikali kupata mapato yake na kujua nani aliyelipa na amelipa kwa kitu gani.

Alisema awali walikuwa na changamoto ya kupokea malipo mengi kutoka taasisi za serikali lakini malipo hayo hayajioneshi yametoka wapi.

Alitumia muda huo kuwasisitiza wahasibu kufuata utaratibu huo na kuhakikisha kabla ya kufanya malipo kufika ZRB kupatiwa namba hiyo ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuweka uwazi kwa wale wanaofanya malipo.

Naye, Ofisa Uhusiano wa bodi hiyo, Badria Attai Masoud, aliziomba taasisi hizo kushirikiana na bodi hiyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na serikali na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.