NA LAYLAT KHALFAN

WAFANYABIASHARA mbalimbali wa soko kuu la Darajani, wameiomba serikali ya Mapinduzi Zanzibar,  kuwapunguzia ukubwa wa  kodi kwa kipindi chote walichokuwa wamekabiliwa na  Corona.

 Walisema kwa hivi sasa kulipa shilingi 60,000 kwa mwezi ni vigumu  kutokana na kuzorota kwa biashara sokoni hapo kufuatia maradhi hayo ambayo takriban nchi zote duniani imekumbwa na kadhia hiyo .

Waliyasema hayo Darajani kwa nyakati tofauti wakati walipokuwa wakizungumza na Mwandishi wa habari wa gazeti hili, ambapo walisema licha ya kuwa milango ya watalii imefunguliwa hapa Zanzibar, lakini nchi za ulaya bado zinasumbuliwa na ugonjwa huo na kutoruhusiwa kuingia nchini.

Mmoja wa wafanyabiashara hao ambae amejikita katika masuala ya viungo (spice), Deogratias Samson,alisema toka kuingia Corona biashara imekuwa mbaya inafikia hatua kwa siku huambulii  hata shilingi huku serikali ikiwa inasubiri kodi yake mapema ifikapo mwisho wa mwezi.

Alisema wananchi wa kawaida si aghalabu kununua bidhaa hizo kwa madai zinauzwa ghali kwa kua imelenga zaidi watalii wanaotoka nchi tofauti duniani.

Abdallah Suleiman, mfanyabiashara wa matunda sokoni, alisema inafikia wakati biashara inarudi kama ilivyo wakati tayari ametumia fedha nyingi kwa ajili ya kununua bidhaa hiyo.

“Matunda dada yangu hayahimili vishindo siku moja ya pili yashanyauka hasara juu ya hasara maana bei ninayonunulia ni kubwa na faida yake siioni wakati mwengine ile pesa ya kununulia pia hairudi”, alisema.