NA KHAMISUU ABDALLAH

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imeukabidhi Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) eneo la hoteli ya Bwawani ili kuifanyia matengenezo na kuona hoteli hiyo inakuwa ya kimataifa.

Imesema ujenzi huo unatarajiwa kuanza mwezi Septemba mwaka huu kwa kuanza na ukumbi wa Salama hall ili uweze kutumika katika shughuli mbalimbali za serikali na kijamii.

Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa aliyasema hayo wakati alipofanya ziara katika hoteli hiyo na mradi wa nyumba za ZSSF Mbweni.

Alisema serikali imeamua kuikabidhi ZSSF kwa ajili ya ujenzi ili kuona eneo hilo linarudi katika haiba yake na linafanya kazi kama ilivyokuwa zamani.

Balozi Ramia alibainisha kuwa tayari imeshatoa kibali kwa ajili ya kuanza kazi ya ujenzi wa eneo hilo na kuona kazi hiyo inafanyika kama ilivyokusudiwa.

Alisisitiza kuwa serikali haijalitupa eneo hilo kwani lina manufaa makubwa katika kuongeza mapato yake kupitia nyanja mbalimbali.

“Lengo letu ni kuona serikali ya awamu ya saba inaaza kulifanyia ukarabati eneo hili na awamu inayokuja italiendeleza na kulimaliza,” alisema.

Alifahamisha kuwa mradi huo ulikuwa na changamoto mbalimbali baada ya kampuni iliyoshinda tenda kushindwa kuuendeleza mradi huo.

Hivyo, alibainisha kuwa wizara ya Fedha itahakikisha inashirikiana na mfuko huo ili lengo lililokusudiwa linafikiwa katika eneo hilo.

Akizungumzia ujenzi wa nyumba za makaazi Mbweni, Balozi Ramia aliutaka mfuko huo kuendelea kubuni miradi mengine ya nyumba za makaazi itakayoleta tija kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Mbali na hayo alizitaka taasisi nyengine zinazosimamia miradi kuiga mfano wa mfuko huo na kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati miradi wanayoianzisha.

Meneja Uwekezaji wa Mfuko huo, Abdul-aziz Ibrahim Iddi alisema pamoja na serikali kuwakabidhi hoteli hiyo lakini hawatoweza kufanya ukarabati eneo lote la hoteli hiyo peke yao na badala yake watashirikiana na taasisi nyengine ambazo zimeshapeleka maombi.

Alizitaja taasisi zilizopeleka maombi hayo kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji na Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA), Manispaa ya Mjini (ZMC) na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) kuona wanashirikiana katika ujenzi huo.