NA KHAMISUU ABDALLAH                

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), inatarajia kutoa leseni kwa wauzaji wakubwa na wasambazaji wa gesi nchini, ili kuhakikisha biashara hiyo inaendeshwa kwa misingi ya usalama.

Imesema kuwa hadi sasa imeshapokea maombi ya wafanyabiashara watano wanaoingiza bidhaa hiyo nchini na wasambaji tisa kwa ajili ya kupatiwa leseni.

Ofisa Uhusiano wa mamlaka hiyo, Hassan Juma Amour, aliyasema hayo wakati akizungumza na gazeti hili Ofisini kwake Kikwajuni.

Alisema, hatua hiyo imefikiwa baada ya mamlaka hiyo kuridhishwa na hatua ya utoaji wa elimu juu ya kanuni ya gesi ya kupikia LPG ya mwaka 2017 na miongozo ya gesi kwa ajili ya kusimamia uendeshaji wa baishara hiyo hapa Zanzibar.

Alisema lengo la mamlaka hiyo kutoa leseni ni kusimamia biashara hiyo na kujua muingizaji na muuzaji wa reja reja anaendesha vipi biashara hiyo na anasimamia kwa misingi ya usalama na viwango vinavyokubalika.

Aidha, alisema ZURA imeona umuhimu wa kutoa elimu kabla ya kusimamia sheria na miongozo, ili kuhakikisha pale zitakapoanza kutumika basi zinafahamika na zinafuatwa.   

“Hivi sasa soko la gesi ya kupikia hapa Zanzibar, limekuwa kwa kasi hivyo mamlaka yetu imeona kunahitajika udhibiti na jambo hilo linahitaji kusimamiwa kwa nguvu zote kama inavyosimamia sekta ya mafuta,” alibainisha.

Alibainisha kuwa, Zanzibar inategemea soko la Tanzania bara kuagiza nishati hiyo ambapo kampuni zinazofanya biashara hiyo ya jumla ni pamoja na V- Gas, Oryx Gas, Oilcom.

Ofisa Hassan, alisema utoaji wa leseni baadae utawahusisha wauzaji wa rejareja ili kuona kila mtu anakuwa na leseni iliyokuwa kisheria.

Akizungumzia wafanyabiashara wauza gesi katika maduka ya vyakula alisema kanuni ya gesi inakataza kuchanganya bidhaa hiyo na bidhaa nyengine kwa usalama wa eneo husika.

“Kigezo kimoja cha kutoa leseni ni lazima kabla ya mfanyabiashara kupewa leseni yake lazima kwanza wakaguzi wakaangalie eneo husika linalohifadhiwa mitungi ya gesi lina hewa ambayo dharura yote ikitokea haisababishi maafa ikiwemo moto,” alisema.

Hata hivyo, alibainisha kwamba mfanyabiashara yoyote ambae atatimiza vigezo vya kupatiwa leseni ya kuendesha biashara hiyo na kukiuka sheria za uendeshaji wa biashara hiyo basi hatopatiwa leseni kwa mara ya pili.

“Mara kwa mara tutafanya ukaguzi ili kujua bado mfanyabiashara anaendeleza masharti aliyopewa ya kuendesha biashara hii kwa mujibu wa leseni yake,” alisema. 

Akizungumzia wafanyabiashara wanaouza bidhaa hiyo katika nyumba alisema wanakwenda kinyume na sheria kwani inakatazwa kuuza bidhaa hiyo kwenye maeneo ambayo hayana uhifadhi nzuri ya mazingira.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Khudhaimat Bakar Kheir, alisema ZURA ina jukumu la kusimamia shughuli za nishati ikiwemo gesi ya kupikia majumbani ili kuona haileti madhara kwa watumiaji.

“ZURA inadhibiti gesi kama inavyodhibiti nishati ya mafuta ikiwemo uingizaji, usambazaji na wauzaji wa rejareja lengo letu ni kuona nishati hii haileti madhara kwa mtumiaji,” alisisitiza.

Hivyo, aliwaomba wafanyabiashara ambao bado hawajapeleka maombi ya kupatiwa leseni kuhakikisha wanaomba leseni ili kuendesha biashara zao kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na mamlaka hiyo katika kusimamia nishati hiyo.