NA ASYA HASSAN

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), imesema Zanzibar haina upungufu wa mafuta ya taa, kwani kuna lita 26,388 ambazo zinatosheleza kwa matumizi ya siku kadhaa hapa nchini.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa kitengo cha mahusiano wa mamlaka hiyo, Hudhaimat Bakar Kheir, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari katika ukumbi wa ofisi hiyo iliyopo Maisara Mjini Zanzibar.

Alisema mafuta hayo yanaweza kutosheleza kwa matumizi ya wananchi kwa siku hizo, huku lita nyengine 600,000 tayari zimeshaagizwa na zinatarajiwa kuwasili nchini wakati wowote.

Sambamba na hayo mkuu huyo alitumia fursa hiyo kuwataka wamiliki wa vituo vya mafuta kutouza bidhaa hizo kwa bei zisizo rasmi na hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kwenda kinyume na bei halali zinazotangazwa na mamlaka hiyo.

Akizungumzia bei ya mafuta hayo alisema mwezi wa Julai mafuta hayo yalikuwa yakiuzwa shilingi 1,800 na mwezi huu wa Agosti yanauzwa shilingi 1,188.

Aidha aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka hiyo endapo kukiwa na tatizo lolote juu ya upatikanaji wa huduma hizo ili waweze kuchukua hatua za haraka.

Naye ofisa uhusiano wa Mamlaka hiyo, Mbarak Hassan Haji, aliwanasihi wananchi kusikiliza maelezo yanayotolewa na ZURA na badala yake kuacha kusikiliza maneno ambayo hayana ukweli yanayotolewa na baadhi ya watu huko mitaani.