NA MWAJUMA JUMA

SHIRIKISHO la soka visiwani Zanzibar (ZFF) limetuma salamu za rambi rambi kwa familia ya aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Jang’ombe, na mdau wa michezo Salum Hassan Turkey aliyefariki usiku wa kuamkia jana.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho hilo iliyosainiwa na Kaimu Katibu wake Ali Ame Vuai, imesema wamesikitishwa sana na taarifa ya kifo chake na kuwataka ndugu na wale wote ambao wameguswa na msiba huokuwa na subira katika kipindi hiki.

Vuai kupitia taarifa yake hiyo alisema Turkey alikuwa mdau mkubwa wa michezo na amesaidia sana klabu pale zilipotaka msaada.

Kwa upande wa timu ya Taifa ya Jang’ombe Katibu wa timu hiyo Said Kindehe amesema kifo chake kimeacha pengo katika klabu yao, kwani kuna mipango mingi aliwapangia katika kipindi hiki.

“Kwa ufupi tumeathirika sana kwani mbali ya kuwa ni mbunge wetu lakini pia alikuwa mfadhili mkuu wa timu yetu kwa kila hali”, alisema.