NA MWANTANGA AME, PEMBA

MKE wa Rais wa Zanzibar, mama Mwanamwema Shein, amewataka wanawake kisiwani Pemba kufanya kila jitihada kuhakikisha wanasaka kura zitakazokiwezesha Chama cha Mapinduzi kinashinda kwenye uchaguzi wa Oktoba 28 mwaka huu.

Mama Shein aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza katika kongamano la wanawake wa Chama cha mapinduzi, lililofanyika katika ukumbi wa Kiwanda cha Makonyo, Chake Chake.

Mama Mwanamwema alisema ili chama hicho kijihakikishie ushindi kwenye uchaguzi huo, wanawake kama jeshi kubwa na muhimu, lazima wapite nyumba kwa nyumba kupiga kampeni ili Dk. Hussein Mwinyi aweze kupata ushindi wa kishindo.

Mama Shein, alisema wanawake ndio kichocheo cha maendeleo ya familia na taifa, kwani wamekuwa katika harakati nyingi za kichocheo cha ukombozi na ni vyema wakaona umuhimu wa kukipigia kura Chama cha Mapinduzi ili Dk. Hussein Mwinyi aweze kushinda.

“Nakubaliana na kaulimbiu ya mkutano huo, ‘Umoja wetu ndio nguvu yetu’, kuna umuhimu mkubwa, kwani vyama vya ASP na TANU viliona umuhimu wa nguvu ya mwanamke na ndio maana kukawa na chombo cha umoja wa wanawake wa Tanzania”, alisema.

Alisema serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein amekuwa akihimiza wanawake kuwa pamoja, ukiwemo wa kuunda vikundi vitakavyowawezesha kupata mikopo.

Alisema pia serikali imejitahidi kuwafikishia huduma za umeme, maji na shughuli nyengine za kijamii, bila ya ubaguzi ikiwa ni hatua ya kuwaondolea usumbufu wanawake kwa vile kukosekana kwa huduma hizo wao ndio wanaotaabika.

Alisema mgombea wa CCM, Dk. Hussein Mwinyi, ameonesha kuwajali wanawake kwa kukubali kuwapa nafasi nyingi za uteuzi, jambo ambalo ni la kupongezwa na kinachohitajika kuona wanajitokeza kwa wingi Oktoba 28 kwenda kupiga kura.

Naye mke wa mgombea wa CCM, Mama Maryam Hussein Mwinyi, amewapongeza wanawake waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali kwa uthubutu wa kuwania nafasi hiyo.