NA HAFSA GOLO

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa  wa Magharibi Kichama, Mohammed Rajab Soud, amesema ushindi wa chama chochote cha siasa unapatikana kwa idadi ya  kura na sio kwa kucheza ngoma au kuhudhuria kwa wingi mikutanoni.

Alieleza hayo wakati akiwanadi wagombea wa majimbo matano ya Wilaya ya Mfenesini kichama katika kiwanja cha Kihinani.

Alisema pamoja na CCM kuwa na wanachama wengi haitosaidia kuleta ushindi  wa kishindo kama watu  hawatojitokeza vituoni kwenda kupiga kura.

 “Nakuombeni vijana itapofika siku ya Uchaguzi Oktoba 28 mwaka huu nendeni nyote mkapige kura msifanye makosa”,alisisitiza.

Nae Mwenyekiti wa Wilaya ya Mfenesini Kichama Kesi Mashaka Ngusa alisema, zipo kila sababu kwa CCM kushinda kutokana na kuwa  na wagombea wenye uwezo na sifa sambamba na idadi  kubwa ya wanachama hai waliojioreshesha katika daftari la kudumu la kupiga kura.

Alisema  sababu nyengine ya kusema ushindi ni lazima kutokana na   chama hicho kimekuwa kikilinda amani na usalama wa nchi sambamba na ndio tegemeo kubwa kwa wananchi waliowengi hasa wanyonge.   

Ngusa aliahidi CCM kuendelea kufuata sheria na kufanya kampeni za kistaarabu wakati wote kikiendelea na kudadi sera na ilani kwa wagombea wake.

Kwa upande wa aliekuwa Mbunge wa jimbo la Mfenesini ambae katika kura za maoni  katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka huu  hazikutosha, Mstaafu Kanali Masoud Khamis aliwataka vijana kutambua kwamba kipindi hichi ni cha kusaka ushindi wa CCM  na sio kuendeleza makundi na malumbano yasio na tija.

“Matabaka hayawezi kuleta ushindi ndani ya chama hichi tuipiganie CCM kwa pamoja na  tuendelee  kudumisha umoja na mshikamano ndio utakaotuvua salama”,alisisitiza.