ABUJA, NIGERIA
WATU 28 wamepoteza maisha katika mripuko wa lori la mafuta katika jimbo la Kogi,nchini Nigeria.
Msemaji wa Idara ya Usalama wa Barabarani nchini humo (FRSC) Bisi Kazeem, alisema watoto tisa ni miongoni mwa watu waliofariki dunia katika ajali hiyo iliyotokea mkabala wa kituo cha kuuzia mafuta katika barabara kuu ya Lokoja-Zariagi.
Gavana wa jimbo hilo,Yahaya Bello alisema ajali hiyo iliyotokea Jumatano,mbali na kusababisha maafa ya binadamu,lakini pia iliharibu idadi kubwa ya magari,majengo na vitu vyengine vya thamani.
Miripuko ya malori na mabomba ya kusafirishia mafuta na gesi imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara nchini Nigeria,taifa la Afrika magharibi lenye utajiri wa bidhaa hizo.
Mapema mwaka jana,makumi ya watu walipoteza maisha katika mripuko wa lori la mafuta katika eneo la Odukpani, jimboni Cross River kusini mashariki mwa Nigeria.
Kadhalika Machi mwaka huu,mripuko wa bomba la gesi uliotokea katika mji mkuu wa kibiashara wa Lagos nchini Nigeria ulipelekea watu 15 kufariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa.