KIGALI,RWANDA
RAIS wa Rwanda Paul Kagame amekanusha kwamba Serikali yake ilimteka Paul Rusesabagina ambaye sasa anashikiliwa nchini humo kwa makosa ya ugaidi na mengineyo.
Rusesabagina ni maarufu duniani kutokana na alivyoonyeshwa katika filamu ya Hotel Rwanda kama shujaa aliyesaidia kuokoa maisha ya mamia ya watu wakati wa mauaji ya halaiki nchini humo.
Katika mkutano na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kutoka mji mkuu wa Rwanda, Kigali, Rais Kagame hakusema wazi namna Rusesabagina alivyokamatwa, lakini alisema kwamba walimfanyia mbinu ya kusafiri kwenda Rwanda kabla ya kukamatwa kwake.
Alisema si kweli kwamba Resusebagina alitekwa na maofisa wa Rwanda nje ya nchi hiyo.
Kigali ilitangaza kumshikilia Resesabagina Agosti 1,na kumwonyesha kwa umma akiwa amefungwa pingu.
Kumekuwa na habari tofauti kwamba Rususebagina alikamatwa na maofisa wa Rwanda katika uwanja mmoja wa ndege nje ya Ubelgiji ambako alikuwa akiishi kwa miaka kadhaa sasa.
Idara ya uchunguzi wa makosa ya jinai ya Rwanda ilieleza kwamba Rusesabagina anakabiliwa na mashitaka kadhaa ikijumuisha ya ugaidi, kufadhili ugaidi, uhaini, utekaji na mauaji.
Rwanda imemshutumu Rusesabagina kwa kushiriki katika mashambulizi ya waasi wa National Liberation Front kusini mwa Rwanda katika mpaka na Burundi mwaka 2018.
Paul Rusesabagina ana uraia wa Ubelgiji lakini alikuwa na hati halali za kuishi Marekani hadi alipokamatwa.
Rais Kagame pia alizungumzia maandamano yaliotokea wiki iliyopita mbele ya ubalozi wa Rwanda mjini Kinshasa nchini DRC, wale waliopanga maandamano hayo walikuwa nyuma ya mpango wa kuharibu uhusiano mzuri wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wiki iliyopita mbele ya ubalozi wa Rwanda mjini Kinshasa kulitokea maandamano makubwa yakishinikiza kwamba balozi wa Rwanda nchini humo Vincent Karega arejeshwe Rwanda kutokana na sababu ambazo hazikufafanuliwa.
Kagame pia alizungumzia uhusiano wa Rwanda na mataifa ya Uganda na Burundi ambayo kwa miaka ya hivi karibuni yamekuwa mahasimu wakubwa wa Rwanda .