TOKYO,JAPAN
WAZIRI Mkuu wa Japan Shinzo Abe na baraza lake la mawaziri wamejiuzulu rasmi, na kusafisha njia kwa mrithi wake kuchukua madaraka, baada ya kuthibitishwa na bunge jana.
Kabla ya kuongoza kikao cha mwisho cha baraza lake, Abe ambaye ndie Waziri mkuu wa Japan aliyedumu madarakani kwa muda mrefu zaidi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa alijitolea mwili na roho kwa ajili ya kuufufua uchumi wa nchi yake, na kuimarisha diplomasia kwa maslahi ya taifa hilo.
Mkuu wa baraza la mawaziri Yoshihide Suga alichaguliwa Jumatatu wiki hii kuwa kiongozi wa chama tawala cha Liberal Democratic, na anatarajiwa kuidhinishwa na bunge kuchukuwa mikoba ya Shinzo Abe aliyetangaza kujiuzulu mwezi uliopita kutokana na matatizo ya kiafya.