NA ZUHURA JUMA

JAMII imetakiwa kuepuka kuchagua viongozi kwa njia ya rushwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ili kujenga jamii iliyobora.

Wakitoa elimu katika shehia mbali mbali za Mkoa wa Kaskazini Pemba, watendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la ActionAid, walisema, kuchagua viongozi bila ya rushwa inawezekana, hivyo watimize wajibu wao. Walieleza kuwa, kuna baadhi ya wagombea hutoa rushwa ili wachaguliwe kuwa viongozi, jambo ambalo sio sahihi kwani huwa sio watendaji wazuri wanaoweza kuleta mabadiliko katika jamii. Walisema jamii inahitaji viongozi imara na wenye kuleta maendeleo, hivyo ni vyema wakachagua viongozi bila kuchukua rushwa, ili kujenga jamii iliyobora zaidi.


“Mnapomchagua kiongozi kwa rushwa, hata akipata uongozi itakuwa hawajali nyinyi kwa sababu amewapa rushwa na ndio sababu wanahama makaazi yao, walisema. Mussa Suleiman Said kutoka shirika hilo alieleza kuwa, ili kujenga jamii iliyobora na yenye maendeleo ni vyema kujiepusha na rushwa.“Rushwa ni adui wa haki, rushwa inadumaza maendeleo, hivyo tuachane nayo, tuchague viongozi bila ya rushwa, hii itatusaidia kupata maendeleo,” alisema. Kwa upande wake, muwasilishaji mada, Biubwa Suleiman Juma, alisema jamii inapochagua viongozi kwa rushwa, viongozi hao hawatakuwa na huruma .