Kilimo cha uzalishaji wa sabuni ya TIBA, HIBA

NA MWANTANGA AME

MGOMBEA wa Rais wa Chama cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib, amesema akiingia madarakani atahakikisha anaimarisha uchumi wa viwanda kwa kuvirejesha vile ambavyo vilikuwapo Zanzibar, ikiwa ni hatua itayokuza ajira kwa vijana.

Khatib, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Zanzibar Leo, juu ya sera ya Chama hicho inazoratajia kutekeleza pindi atapoingia madarakani.

Alisema Zanzibar ilikuwa na viwanda vingi vidogo vidogo, lakini vilikufa kutokana na uchumi kushuka, lakini atapoingia madarakani atahakikisha anavifufua, ili viweze kupunguza tatizo la ajira.

“Mimi nilikuwa mwajiri wa serikali na nikuwa nafanyakazi katika viwanda vidogo vidogo Amaani, najua nilivyoweza kufaidika na uwepo wa viwanda vile kwa ajira tuliyoipata sasa nikiingia madarakani nitavirejesha vyote” alisema.

Khatibu akivitaja viwanda hivyo, alisema ni pamoja na cha kutengeza sabuni ya kuogea na kufulia, ikiwemo ya TIBA na HIBA, kiwanda cha mafuta ya nazi, viatu, masufuria ya kutumia madini ya aluminiamu na cha  Samli.

Alisema alisema atavirudisha viwanda hivyo kwa kuongeza idadi ya upandaji wa minazi ikiwa ni hatua itayovifanya viwanda vya mafuta kukuza idadi kubwa ya raslimali ya kufanikisha uzalishaji huo.

Alisema eneo  jengine ambalo wanapanga kulitekeza ni ukuzaji ya utalii kwa kuongeza idadi yao kutoka watalii 500,000 hadi 800,000, huku wakiimarisha huduma zao, ikiwemo za uanzishaji ujenzi wa barabara maeneo ya fukwe, ili iwe rahisi kutembelewa kwa usafiri wa vyombo vya moto.

Alisema katika eneo hilo pia wanakusudia kukuza utalii wa ndani, kwa kuyatangaza zaidi maeneo ya kihistoria, ikiwa ni hatua itayoongeza idadi ya watalii wataoingia nchini.

Eneo jengine ambalo alisema atalisimamia akiwa Rais wa Zanzibar ni pamoja na ukuzaji wa biashara, kwa kuondoa msongomano wa makontena katika bandari ya Zanzibar.

Akizungumzia juu ya raslimali ya mafuta na gesi asilia, Khatib, alisema chama chake kitahakikisha kinasimamia vyema sera ya CCM ya kuendeleza suala la utafiti wa Nishati hiyo.

Aliipongeza serikali ya Zanzibar kwa jitihada ilizozifanya za kuliondoa suala hilo katika mambo ya Muungano, ambapo hivi sasa tayari limeonesha muelekeo mzuri  wa kuwapo kwa mikataba mbali mbali iliyofungwa na itayotaka kufanyiwa kazi.

Kutokana na hali hiyo Mgombea huyo, alisema Chama chao kitahakikisha kinapata ushindi katika uchaguzi mkuu ujao, ili waweze kuteleza waliojipangia kwa maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.