NA MWAJUMA JUMA

CHAMA Cha Alliance for Democratic Change (ADC) kinatarajia kuzindua kampeni zake leo visiwani Zanzibar za kumnadi mgombea wao Queen Sendiga ambae anawania nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa chama hicho Doyo Hassan Doyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba uzinduzi wa kampeni hizo utafanyika katika viwanja vya Mnazimmoja saa 10:00 za jioni.

Doyo alisema wameamua kuzindua kampeni zao kutokana na kuwa Zanzibar ni sehemu tukufu katika mipango ya kisiasa hivyo kuendelea kuienzi heshima hiyo.

Hata hivyo alisema lengo la mkutano na waandishi wa habari ni kuwapa taarifa ya uzinduzi wa mikutano yao ya kampeni pamoja na kuwa ni mwendelezo wa taarifa kwa watanzania kwa namna ambavyo chama chao kimejipanga kwa mwaka huu wa uchaguzi 2020.

Alisema mbali na kuzindua kampeni, pia watazindua ilani yao ya uchaguzi ya 2020/2025 ambayo imebeba mambo matatu makubwa yenye maslahi kwa nchi hiyo.

“Tunakwenda kuwapelekea watu ilani ambayo itazalisha ajira za kutosha na itakayosababisha watu waishi kwa amani na utulivu,” alisema Doyo.

Sambamba na hayo, alisema kuwa chama chao kinalaani kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa zinazochochea uvunjifu wa amani nchini.

Alisema tayari wameanza kushuhudia kauli za uchochezi kwa viongozi hao ikiwa chama cha ACT Wazalendo ambao walisema kuwa iwapo wagombea wao watawekewa pingamizi hakutakuwa na uchaguzi wa amani.

Aidha Doyo alisema chama chake ni muathirika wa jambo hilo la kuwekewa pingamizi wagombea wake 39 wa nafasi mbali mbali za uongozi Tanzania Bara lakini hawajatamka neno lolote ambalo litaashiria kuleta vurugu na kuvunja amani na utulivu iliyopo katika nchi.

Hata hivyo alisema kuwa wamepanga kufanya kampeni rahisi na zisizo na gharama na kuahidi kutomchangisha mtu kama ambavyo baadhi ya vyama vya siasa vinavyofanya.