NA KHAMISUU ABDALLAH

KITENDO cha kumtishia mwenziwe kumkata kichwa akiwa na msumeno na panga kwa kumtuhumu kuwa mchawi kimemsababishia Ali Shaaban Mwinyi kufikishwa mahakamani.

Mshitakiwa huyo mwenye umri wa miaka 50 mkaazi wa Fuoni Michenzani wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Suleiman Jecha Zidi na kusomewa shitaka lake na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai.

Hati ya mashitaka iliyowasilishwa mahakamani hapo ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kutoa lugha za vitisho kinyume na kifungu cha 71 (1) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Ali alidaiwa kuwa bila ya halali akiwa ameshikilia msumeno na panga alimtishia Ali Issa Sharif, kwa kumwambia kuwa yeye ni mchawi na popote atapompata atamkata kichwa kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Tukio hilo alidaiwa kulitenda Juni 30, mwaka huu saa 1:30 asubuhi huko Fuoni Michenzani wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana kwa madai kuwa ana familia inayomtegemea.

Mwendesha Mashitaka Koplo Vuai aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo tayari umeshakamilika, na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.

Mahakama iliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 12, mwaka huu, na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo na kumtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 50,000 za maandishi na mdhamini mmoja atakaemdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi pamoja na kuwasilisha kitambulisho kinachotambulika.