NA MARYAM HASSAN
KIJANA aliyemtishia mwenzake Panga amehukumiwa kulipa faini ya shilingi 150,000 baada ya kusomewa kosa lake na kukubali.
Kijana huyo ni Mohammed Mayala Fungameza (33) mkaazi wa Dunga wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja, amepewa adhabu hiyo na Hakimu Johari Ali Makame wa mahakama ya mwanzo Mwera.
Hakimu huyo alisema endapo mshitakiwa atashindwa kulipa faii hiyo atumikie Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja na haki ya rufaa imetolewa kwa upande usioridhika na adhabu hiyo.
Hati ya mashitaka ya mshitakiwa huyo, imesomwa na Koplo Khadija Abdalla, na kudai kuwa mshitakiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kufanya kitendo kinachoweza kuleta uvinjifu wa Amani kinyume na kifungu cha 73(1)(a)na (b) sheria nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.
Alidai kuwa tukio hilo ametenda Semptemba 20 mwaka jana majira ya saa 6:00 za mchana huko Dunga wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.
Mshitakiwa alitenda kitendo cha kuleta uvunjifu wa Amani kwa kumtishia panga Abdul Helef Khamis kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Aliposomewa shitaka lake mshitakiwa huyo alikubali na kuiomba mahakama kumsamehe kwa sababu hasira ndizo zilizopelekea kufanya kitendo hicho.