NA HABIBA ZARALI

OFISA Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Mohamed Nassor Salim, amesema mafunzo ya ualimu yaliyotolewa na mradi wa ‘Elimu Bora’ chini ya shirika la Aga Khan Foundation, yameleta faraja kwa kuongeza wigo wa kutoa huduma ya elimu ya maandalizi. Alisema mradi huo ambao umefadhiliwa na shirika la Comic Relief la Uingereza, umeongeza walimu wenye umahiri wa kuwasaidia watoto wa maandalizi kujifunza kwa ufanisi kulingana na mtaala wa serikali.

Alieleza hayo wakati akizungumza katika mahafali ya nne ya ualimu wa maandalizi wa Madrasa Early Childhood yaliyofanyika uwanja wa kufurahishia watoto Tibirinzi Chake-Chake.

Alisema kwa upande wa skuli za maandalizi  za vijijini zinakabiliwa na changamoto nyingi hasa katika maeneo yaliyo na masafa marefu na skuli za msingi  ikiwemo madarasa na vifaa vya kujifunzia na kufundishia lakini kuwepo kwa miradi kunasaidia kutatua matatizo yanayowakabili.

“Wito wangu kwenu ni kuyatekeleza kwa vitendo mafunzo mliyoyapata katika kuandaa madarasa rafiki na jumuishi yaliyosheheni vifaa, hali ambayo  itawajengea heshima nyinyi kama walimu, skuli zenu na jamii kwa ujumla,” alisema.