LA PAZ, BOLIVIA
TAKRIBAN watu saba wamefariki na wengine watano kujeruhiwa baada ya basi dogo kugongana na lori la takataka magharibi mwa Bolivia, taarifa ya polisi ilisema.
Kamanda wa polisi wa jiji la El Alto, Ismael Villca, aliambia wanahabari wa eneo hilo kwamba ajali hiyo ilitokea Ijumaa majira ya asubuhi wakati lori la kubeba mzigo mkubwa na basi ndogo iliyokuwa imebeba abiria kadhaa ilianguka kwenye barabara kuu inayounganisha La Paz na Desaguadero.
Taarifa zaidi zilisema kuwa huenda magari hayo yote yalikuwa yakienda kwa mwendo kasi.
“Polisi na wazima moto wa Bolivia walifika katika eneo la tukio kusaidia kuondoa watu waliokwama kwenye basi hilo, na kuhamisha manusura katika vituo vya matibabu vya eneo hilo”, ilisema taarifa hiyo.
Picha kutoka kwa vyombo vya habari vya nchi hiyo, zilionyesha jinsi mbele ya basi hilo dogo ilivyokuwa imeharibiwa kabisa baada ya kugonga lori kubwa.
Mkuu wa polisi alisema uchunguzi zaidi wa ajali hiyo unaendelea.