NA MARYMA SALUM, PEMBA

MAHAKAMA ya Mkoa Chake Chake, imempandisha kizimbani mzee Ali Mohamed Nassor 60 wa Mgelema Wilaya ya Chake Chake, kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye miaka 16 ambaye hajapata kuolewa.

Akisoma shitaka hilo Mwendesha Mashitaka kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Mohamed Ali Juma, mbele ya Hakimu  wa mahakama hiyo, Luciano  Makoye Nyengo, alidai kuwa mtuhumiwa  anakabiliwa na makosa manne ambayo aliyafanya kwa  nyakati  tofauti.

Ilidaiwa kwamba kosa la kwanza kwa mtuhumiwa huyo, mnamo Agosti  mwaka huu majira ya saa 12:00 jioni, bila halali na bila ridhaa  ya kaka yake alimtorosha  mtoto wa kike mwenye miaka 16, kumpeleka makaburini Mgelema.

Kufanya hivyo ni kosa kinyume na kifungu cha 113(1) (a) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018.

Ilidaiwa kuwa mtoto huyo, alikuwa akipita njiani kwenda nyumbani kwao, na ndipo mtuhumiwa alipomchukuwa na kumpeleka kwenye maeneo hayo.

Kosa la pili  kwa mtuhumiwa  ilidaiwa  ya mwezi Januari  mwaka huu, baada ya kumtorosha alimbaka, jambo ambalo  ni kosa kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) (e) na kifungfu cha 109 (1) cha sheria hiyo .

Kosa la tatu , ilidaiwa  kuwa  mtuhumiwa  huyo, mnamo  Agosti 9 mwaka huu  majira ya saa 6:30 mchana katika shehia ya Mgelema, bila halali alimtorosha mtoto huyo jambo ambalo ni kosa.

Kosa la nne kwa mtuhumiwa huyo, baada ya kutorosha alimbaka mtoto huyo, ambapo ni kosa kinyume na kifungu cha 108 (1) (2) (e) na 109 cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar.

Mara baada ya kumaliza kumsomea shitaka, hakimu Luciano alimuuliza mtuhumiwa ikiwa ana lolote, na kukana mashitaka hayo na kisha kupelekwa rumande hadi Septemba 8 mwaka huu.