NA MARYAM HASSAN
KITENGO cha kupambana na dawa kulevya kimempandisha katika Mahakama ya mkoa Vuga kijana Zahor Salum Abdallah, ambae alipatikana akiwa anasafirisha dawa za kulevya.
Kijana huyo alipandishwa mahakamani mbele ya Hakimu Valevtina Katema na kusomewa shitaka lake na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Ahmed Mohammed.
Wakili huyo alidai kwamba mshitakiwa huyo alipatikana akiwa anasafirisha dawa za kulevya kinyume na vifungu 15(1)(b) (11) cha sheria nambari 9 ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho chini ya kifungu cha 11 (a) sheria nambari 12 ya mwaka 2011.
Kosa hilo alidaiwa kutenda Juni 19, mwaka jana majira ya saa 8:20 za mchana huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Aman Karume Zanzibar.
Alidai kwamba mshitakiwa alipatikana akiwa anasafirisha maboksi mawili ndani yake mkiwa na dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi zilizokuwa zimefungwa katika karatasi ya mga’ro zenye uzito wa gramu 48 kitendo ambacho ni kosa kisheria.
Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani kwa ajili ya kusikilizwa ushahidi dhidi ya shauri lake, lakini liliahirishwa kutokana na Hakimu husika hayupo na kutakiwa kurudi Septemba 24, mwaka huu.
Aidha Hakimu huyo aliwaonya mashahidi hao na kuwataka kufika tarehe hiyo kwa ajili ya kuja kutoa ushahidi dhidi ya mshitakiwa huyo.
Kabla ya kuahirishwa upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi wawili, na kueleza kuwa wako tayari kutoa ushahidi