Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya wanasiasa nchini wametakiwa kuhubiri sera za vyama vyao za maendeleo ya nchi hii, badala ya kuanza kutishia kuvunja Muungano wa Tanzania kwani haukuundwa kwa porojo la mtu mmoja bali yalikuwa ni maamuzi ya wananchi wa pande mbili.
Msimamo huo umetolewa jana na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mzee Ali Ameir Mohamed akiwa kijijini kwake huko Donge Kichavyani Mkoa wa Kaskazini Unguja, kufuatia matamshi ya wanasiasa wanaowataka wananchi Zanzibar kuingia mitaani ikiwa upinzani hautangazwa kushinda.
Mzee Ameir alisema wanasiasa wenye mitazamo hiyo wana fikra duni na asiyejua mantiki na dhana ya demonrasia na ndio maana wanawaza kuvuruga Amani, jambo ambalo kwa Tanzania chini ya Muungano halitaweza kutokea.
Alieleza kuwa Taifa linaloitwa Tanzania halikuachwa na wakoloni na ni lazima watambue gharama zipi au uzito wa kiasi gani uliobebwa na wasisi wake hadi kuundwa kwa Taifa jipya lililowaunganisha watanzania wanaofikia milioni sitini sasa.
Alisisitiza kuwa ikiwa nchi nyingi za Muungano bado zinadumu yakiwemo Mataifa ya Uingereza , Nigeria ,Ujerumani, Afrika Kusini ma Marekani, hayupo mtu atakayesimama hadharani akausambaratisha Muungano wa Tanzania.
“Wanasiasa wamezaliwa na kuikua Tanzania ikiwa imara na salama chini ya Muungano huu. Nao wataishi ,watazeeka na siku moja watazikwa kwa heshima kwenye mikono ya Muungano kama ilivyotokea kwa kina Mwalimu Julius Myeree ,Mzee Abeid Karume, Aboud Jumbe Benjamin Mkapa, Sheikh Thabit Kombo na Titi Mohamed” alisema .