NA ASIA MWALIM

ABRAHMAN Juma Issa (23) mkaazi wa Kinuni Wilaya ya Magharibi ‘B’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, amefikishwa Mahakamani akikabiliwa na mashitaka mawili ya usalama barabarani ikiwemo kuendesha chombo cha moto ikiwa hana leseni ya njia.

Mshitakiwa huyo alisomewa shitaka hilo likiwa la kwanza ambapo kufanya hivyo ni kinyume na kifungu cha 35 (1) (2) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Huku shitaka la pili likiwa ni kuendesha chombo cha moto barabarani ikiwa hakina bima, kufanya hivyo ni kinyume na kifungu cha 3(1)(2) sura ya 136 sheria za bima za Zanzibar.

Alifkishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Mohammed Ali Haji na kusomewa mashitaka yake na muendesha mashitaka kutoka kituo cha Polisi Koplo Rajab Mussa.

Kwa mujibu wa muendesha mashitaka huyo, alidaiwa kuwa makosa yote mawili aliyatenda Agosti 14 mwaka huu majira ya saa 6:15 mchana huko Kinuni Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Mshitakiwa huyo alipatikana barabarani na gari yenye namba za usajili Z. 987 EX P/V akitokea upande wa Kinuni Skuli akielekea Magogoni

Kijana huyo aliposomewa mashitaka yake aliyakubali na akiomba kusamehewa makosa yake Mahakamani hapo, huku upande wa mahakama ulimtoza faini ya 20,000 au kutumikia miezi miwili endapo akishindwa kulipa faini hiyo kwa kosa la kwanza na kupewa onyo kwa kosa la pili.

Hata hivyo, Abulrahmani aliweza kulipa faini hiyo ili kujinusuru na adhabu hiyo na kuahidi kutorejea tena kosa alilopewa onyo.