NA HUSNA SHEHA

KIJANA aliyedaiwa kuchukua gari isiyo ya kwake na kwenda nayo Mwachealale amepandishwa katika mahakama ya wilaya Mahonda kujibu tuhuma hizo.

Kijana huyo, Makame Hashim Makame (30) mkaazi wa Kihinani, ambae alipanda mahakamani hapo mbele ya Hakimu Nyange Makame Ali, akiwa mahakamani hapo alisomewa shitaka lake na wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Ali Juma.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kupatikana akiwa gari   ya Hamad Khatib Ali aina ya “Coaster” yenye namba za usajili Z.308 FR bila ya ruhusa yake, kutoka Bububu Kihinani na kwenda nayo huko Mwachealale, jambo ambalo ni kosa kisheria.

Kwa mujibu wa hati inaeleza kuwa kitendo cha kuchukua gari bila ya ruhusa ya muhusika ni kosa kinyume na kifungu cha 138 (1)(3) cha sheria ya usafirishaji barabarani namba 7 ya mwaka 2003, sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kutenda tuhuma hiyo Febuari 27 mwaka huu, baina ya saa 6:00 na 8:00 usiku huko Mwachealale Wilaya ya Kaskazini ‘B’Unguja.

Baada ya kusomewa shitaka lake mshitakiwa alikataa kosa, na kuiomba mahakama impatie dhamana ombi ambalo halikua na pingamizi kwa pande zote mbili.