NA KHAMISUU ABDALLAH
ABDALLA Salum Ame (26) umaarufu dula teri mkaazi wa Mwanyanya amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe akikabiliwa na tuhuma za shambulio.
Mshitakiwa huyo akiwa mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume alisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Salum Ali, ambapo alidai mshitakiwa huyo alimshambulia Rasam Abeid Ussi, kwa kumpiga ngumi ya jicho la upande wa kushoto na pua na kumsababishia kupata maumivu mwilini mwake.
Kosa la shambulio la kuumiza mwili ni kinyume na kifungu cha 230 cha sheria namba 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.
Koplo Salum alidai kuwa mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Disemba 29, mwaka jana, majira ya saa 6:33 mchana huko Bububu skuli Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikataa na kuiomba mahakama impatie dhamana huku upande wa mashitaka ukidai kuwa tayari upelelezi wa shauri hilo umeshakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha mashahidi.
Mahakama ilikubaliana na ombi la upande wa mashitaka na kuiahirisha kesi hiyo hadi Septemba 7, mwaka huu, na kuamuru upande wa mashitaka kuwasilisha mashahidi siku hiyo.
Hakimu Nassem, alimtaka mshitakiwa huyo kujidhamini mwenyewe kwa shilingi 100,000 za maandishi na kuwasilisha wadhamini wawili ambao kila mmoja atamdhamini kwa kima hicho hicho cha fedha za maandishi na kuwasilisha vitambulisho vyao vyovyote vinavyotambuliwa na serikali.
Mshitakiwa huyo alikamilisha masharti hayo na yupo nje kwa dhamana, hadi tarehe nyengine aliyopangiwa mahakamani hapo.