NA KHAMISUU ABDALLAH

MAHAKAMA ya Wilaya Mwanakwerekwe imeiharisha kesi inayomkabili Khamis Shkeli Masoud (50) mkaazi wa Chuini Wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja hadi Septemba 28 mwaka huu.

Hakimu Mummin Ali Juma, aliiharisha kesi hiyo baada ya ombi lilotolewa na upande wa mashitaka kuomba kuhairishwa na kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kuwasilisha shahidi.

Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na mashitaka mawili ya wizi baada ya kuaminiwa kinyume na kifungu cha 274 (7) (b) cha sheria namba 6 ya mwaka 2004 sheria za Zanzibar.

Mwendesha Mashitaka Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) Said Ali alidai kuwa siku na tarehe isiyofahamika mwaka 2013 saa 5:00 asubuhi huko Nyerere mshitakiwa huyo aliaminiwa na kukabidhiwa fedha taslimu shilingi 15,000,000 mali ya Kiumbwa Makame Mbaraka.

Mshitakiwa huyo alidaiwa kutapeli pesa hizo kwa kudai kumnunulia gari aina ya basi (Rosa) kitendo ambacho hakukifanya jambo ambalo ni kosa kisheria.

Aidha kosa jengine alidaiwa kuwa alijiipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambapo siku isiyofahamika mwaka huo huo majira ya saa 12:00 jioni huko Nyerere aliaminiwa na kukabidhiwa shilingi 12,000,000 na malalamikaji huyo kwa lengo la kutoa gari hiyo Bandarini Malindi Unguja kitendo ambacho hakujikifanya.