MAOFISA wa uhamiaji nchini Marekani, wamemkamata mwanamke mmoja anayeshukiwa kutuma kifurushi kilicho chenye sumu aina ya ricin ndani yake ambacho alilenga kimfikiwe rais wa nchi hiyo Donald Trump.

Mwanamke huyo ambaye hajatajwa jina alikamatwa kwenye mpaka huko Buffalo, New York, akijaribu kuingia Marekani akitokea Canada na ameripotiwa kuwa na silaha.

Mnamo Septemba 20 mwaka huu, barua inayosadikiwa kuwa na sumu kali inayoaminika kuwa ilitoka nchini Canada kwenda ikulu ya White House kwa rais Donald Trump, taarifa hilo ni kwa mujibu wa mashirika ya wapelelezi nchini Marekani.

sumu

Barua hiyo iligunduliwa katika kitengo cha ukaguzi wa vifurushi vya barua katika ikulu ya White House mnamo Septemba 20 mwaka huu na kwenda kuifanyia uchunguzi unga uliomo kwenye barua hiyo.

Shirika la upelelezi la Marekani (FBI) na maofisa wa ulinzi wa siri wanachunguza barua hiyo ilitumwa kutoka wapi na ikiwa kuna nyengine zilitumwa kupitia huduma za posta za Marekani.

Serikali ya Trump haijasema chochote kuhusu shambulizi la sumu hiyo, huku shirika la upelelezi nchini Marekani (FBI), likisema kuwa kwa sasa hakuna tishio linalojulikana kwa usalama wa umma.

“Wakati huu hakuna tisho linalofahamika la usalama kwa umma”, FBI iliiambia televisheni ya CNN katika taarifa huku ofisa mwengine akilieleza gazeti la New York Times kuwa wachunguzi wanaamini kifurushi hicho kilitumwa kutoka Canada.

Mshukiwa huyo anashukiwa ambaye hakutajwa jina huenda alituma sumu hiyo pia huko Texas, kwenye gereza na ofisi ya maofisa wa polisi. Taarifa ya Shirika la habari CNN limeeleza.

Idara ya polisi ya Canada-The Royal Canadian Mounted Police (RCMP) ilisema kuwa inashirikiana kwa pamoja na FBI kuchuguza barua “inayoshukiwa iliyotumwa katika ikulu ya White House”.

Sumi ya ricin nini? Ricin huzalishwa kutokana na usindikaji wa maharagwe ya castor, mmea unaotoka katika familia ya Euphorbiaceae, mbegu za mmea huo ndizo zinazotumika kutengeneza sumu.

Ni sumu hatari, ambayo ukimeza, kuvuta harufu yake au kudungwa sindano, kunaweza kusababisha kichefu chefu, kutapika, kutokwa na damu sehemu mbalimbali mwilini na kuzuia viungo muhimu vya ndani kukosa kufanya kazi na hatimaye kifo.

Hakuna dawa ya kuikata makali sumu ya ricin na kwamba mtu akishambuliwa na sumu hiyo anaweza kufariki baada ya kati ya saa 36 hadi 72, kulingana na kiwango cha dawa, kwa mjibu wa Kituo cha Marekani cha kudhibiti na Kuzuia magonjwa (CDC).

Ricin ishawahi kutumiwa kufanya mashambulio ya kigaidi na inaweza kutengenezwa kuwa silaha kwa mfumo wa unga, gesi au chembe chembe.

Majengo ya ikulu ya White house na majengo mengine ya serikali kuu ya Marekani yameshawahi kulengwa kushambuliwa kwa kutumia sumu ya aina hiyo miaka iliyopita.

Mnamo mwaka 2014, mwanaume mmoja kutoka Mississippi alihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa kutuma barua iliyokuwa na poda ya sumu ya ricin kwa rais Barack Obama.

Miaka minne baadaye, mwaka 2018, mwanajeshi wa zamani wa kikosi cha majini cha Marekani alishitakiwa kwa kutuma sumu hiyo katika ofisi za makao makuu ya jeshi la Marekani-Pentagon na ikulu ya White House.