TRIPOLI,LIBYA

SHIRIKA la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema maelfu ya wahamiaji waliokuwa wakikimbilia barani Ulaya walikamatwa na kurudishwa katika pwani ya Libya mwaka huu.

Pia walipotezwa kwa nguvu baada ya kuondolewa kwenye vituo vya kuwaweka wakimbizi ambavyo sio rasmi vinavyoendeshwa na wanamgambo wanaoshirikiana na serikali ya Libya inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ya mjini Tripoli.

Katika ripoti mpya ya shirika hilo, pia ilielezwa kwamba mamlaka kinzani nchini Libya iliyoko mashariki mwa nchi hiyo iliwaondowa kwa nguvu maelfu ya wahamiaji bila ya kufuata taratibu au kuwapa nafasi wakimbizi hao kutetea kurudishwa walikotoka.

Amnesty International linasema kiasi wahamiaji 8500 wakiwemo watoto na wanawake walikamatwa na kurudishwa nchini Libya kati ya mwezi Januari na Septemba.