NEW DELHI, INDIA
SHIRIKA la Amnesty International limesema limesimamisha shughuli zake nchini India baada ya akaunti zake za benki kufungwa katika kile kilichotajwa kuwa ni hatua ya serikali kulipiza kisasi.
Katika taarifa, shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema limegundua kuwa akaunti zake za benki zilifungwa mnamo Septemba 10.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, kufungwa kwa akaunti hizo kumesimamisha kabisa shughuli za shirika hilo.
Amnesty International ililazimika kuwaachisha kazi wafanyakazi wake nchini India na kusitisha shughuli zake nchini humo.
Serikali ya India inadai kuwa Amnesty International imekuwa ikipokea ufadhili wa fedha kinyume cha sheria.
Amnesty India hivi karibuni iliibua maswali kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki wakati wa ghasia zilizotokea New Delhi mwezi Februari na katika jimbo la Kashmir linalosimamiwa na India.