TRIPOLI, LIBYA

SHIRIKA la kimataifa la utetezi wa haki za bindaadamu la Amnesty International limeulaumu Umoja wa Ulaya kwa ukiukwaji wa haki za wakimbizi na wahamaji nchini Libya, ambao mateso yao yalizidishwa na vizuizi vilivyotokana na kukabiliana na janga kubwa la virusi vya corona.

Ripoti mpya ya shirika hilo lenye maskani yake mjini London, Uingereza imeukosoa Umoja wa Ulaya na mataifa wanachama wake, kwa kuiunga mkono serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli .

Pia umoja huo uliukosoa kwa kitendo cha kuweka ulinzi katika eneo la pwani ya Libya kwa lengo la kuzuia wakimbizi na wahamiaji na hatimaye kuwarejesha Libya.

Shirika la Amnesty International limesema wamekuwa wakipelekwa katika vituo vya kuwahifadhi ambako wanawekwa kizuizini kiholela na bila ya ukomo jambo ambalo shirika hilo linaeleza kuwa si la kiutu.