NA MARYAM HASSAN

HAKIMU wa Mahakama ya Mkoa Mwera, Said Hemed Khalfan, amemnyima dhamana Hafidh Juma Bakari (42) mkaazi wa Mwera Pongwe baada ya kosa lake kuwa halina dhamana na kuamuru kupelekwa rumande kwa muda wa wiki mbili.

Hati ya Mashitaka iliyosomwa na Wakili wa serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Ayoub Nassor Sharif, alidai Hafidh alipatikana na kosa hilo Juni 15, mwaka jana, majira ya saa 3:00 za asubuhi huko Mwera Kiongoni wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.

Hafidh anadaiwa kujaribu kumuingilia mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 15 aliyechini ya uangalizi wa wazazi wake jambo ambalo ni kosa kisheria, kwani ni kinyume na kifungu cha 111 (1) sharia nambari 6 ya mwaka 2018 sheria za Zanzibar.

Hivyo mshitakiwa amepelekwa rumande hadi Septemba 28 mwaka huu kesi yake itakapoanza kusikilizwa ushahidi kwa sababu upande wa mashitaka umekamilisha upelelezi.