NA KHAMISUU ABDALLAH

MKAAZI wa Mtendeni wilaya ya Mjini Unguja amekamatwa na askari polisi wa usalama barabarani akiwa amelewa huku akiendesha gari.

Mshitakiwa huyo alitambulika kwa jina la Ikram Ali Othman mwenye umri wa miaka 23 ambaye alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume na kusomewa shitaka linalomkabili na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Vuai Ali Vuai.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa mshitakiwa huyo alipatikana na kosa la kuendesha chombo cha moto akiwa amelewa ni kinyume na kifungu cha 123 (1) (b) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Ikram alidaiwa kuwa Agosti 30 mwaka huu saa 12:35 asubuhi huo Mazizini akiwa dereva wa gari yenye namba za usajili Z 215 JL P/V akitokea Mbweni kuelekea Migombani alipatikana akiendesha gari hiyo barabarani akiwa amelewa.

Koplo Vuai alidai mshitakiwa huyo alishindwa kuiongoza nyema gari yake na baada ya kupimwa alipatikana akiwa na ulevi wa kiwango 082.4 100/ml kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama impunguzie adhabu kwa madai kuwa hatorejea tena kosa hilo.

Hakimu Nassem alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 100,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa miezi mitatu.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo.