NA LAILA KEIS

MSHITAKIWA Ablillah Haji Juma (35), mkaazi wa Mwera Unguja, amefikishwa Mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe kwa makosa mawili ya usalama barabarani ikiwemo kushindwa kusimama aliposimamishwa na askari Polisi.

Mshitakiwa huyo akiwa mbele ya Hakimu Nassem Faki Mfaume, alisomewa shitaka hilo na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Salum Ali, alisema kufanya hivyo ni kinyume na kifungu cha 141 (1) (a) Cha sheria namba 7 ya mwaka 2003, sheria ya Zanzibar.

Ambapo shitaka la pili lilikua ni kutovaa sare ya udereva wakati wa kazi, kufanya hivyo ni kinyume na kifungu cha 60 (1) (g) (2, sheria ndogo ndogo za magari ya biashara ya mwaka 2005, zilizofanywa chini ya kinyume na kifungu 80 sheria nambari 7 ya mwaka 2005 sheria za Zanzibar.

Mahakama ilidai kuwa, mshitakiwa huyo alitenda kosa hilo Agosti 23, mwaka huu, saa 10:29 jioni maeneo ya Amani Wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja, kwenye mzunguko wa njia.

Ilidaiwa kuwa, aliendesha Gari ya abiria inayokwenda njia namba 538, yenye namba za usajili Z737 CB, akitokea upande wa Welezo kuelekea Mwanakwerekwe, alifanya makosa hayo mawili ikiwa ni kosa kisheria.

Abdillah alisomewa shitaka hilo ambalo amekubali na kuiomba Mahakama imsamehe, ombi ambalo lilikataliwa Mahakamani hapo, kwa kumuona ni mkosa kisheria na kumtaka kulipia faini ya shilingi 20,000 au kutumikia Chuo Cha Mafunzo kwa muda wa miezi miwili.

Mshitakiwa alilipa kiasi hicho ili ajinusuru kwenda kutumikia Chuo cha Mafunzo, kilichopo Kilimani mjini Unguja kwa muda huo aliopangiwa.